

15 April 2025, 5:41 pm
Eneo la Nzuguni mpaka sasa lina Visima Tisa vilivyokamilika ambavyo vina uwezo wa kuzalisha maji wastani wa lita milioni Ishirini kwa siku.
Na Yussuph Hassan.
Waziri wa Maji Mhe Juma Aweso amesema licha ongezeko la watu katika jiji la Dodoma lakini Wizara hiyo imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto ya maji ikiwa ni sehemu ya mkakati wa wizara hiyo.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maji Mhe Juma Aweso wakati wa halfa ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji safi nzuguni awamu ya pili uliofanyika katika ofisi za mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mkoa wa Dodoma Duwasa ambapo mamlaka hiyo imeingia mkataba na mkandarasi Bahaji Construction work wenye thamani ya shilingi Bilioni 5.6.
Mhe Juma Aweso amesema wizara hiyo haitakuwa kikwazo katika kuhakikisha wakazi wa Dodoma wanapata Maji safi na salama.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 ambapo zaidi ya wananchi laki moja na Elfu ishirini na tatu watanufaika.
Kwa upande wake Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini Mhe Antony Mavunde amesema zoezi la utiaji saini huo ni sehemu ya utatuzi wa changamoto ya maji katika jiji la Dodoma kutokana na uhitaji wa huduma hiyo kwa baadhi ya maeneo yenye Mgao.
Itakumbukwa kuwa Eneo la Nzuguni mpaka sasa lina Visima Tisa vilivyokamilika ambavyo vina uwezo wa kuzalisha maji wastani wa lita milioni Ishirini kwa siku ambapo hadi kukamilika kwa awamu ya pili ya mradi huu itasaidia kuongeza hali ya uzalishaji maji kutoka lita milioni 81 hadi 90 kwa siku sawa na ongezeko la asiliami 30 kutoka kwenye chanzo hicho.