

19 March 2025, 5:51 pm
Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya mifugo ili kuhakikisha wafugaji wanapata mbegu bora za malisho na uhakika wa chakula cha mifugo.
Na Mariam Kasawa.
Wakati kilio kikubwa cha wafugaji nchini kikiwa ni ukosefu wa malisho unaosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, Mpwapwa wamepata mwarobaini wa changamoto hiyo.
Changamoto hiyo imetatuliwa baada ya kukamilika ujenzi wa ghala jipya la kisasa la kuhifadhi malisho ya mifugo wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma.
Ujenzi wa ghala hilo umegharimu Sh219.7 milioni ambalo linatarajia kuongeza tija kwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (Taliri) na wafugaji.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dk Asimwe Rwiguza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ilipotembelea mradi huo, amesema ghala hilo litaisaidia Taliri kuhifadhi malisho kwa muda mrefu, kupunguza upotevu na kulinda ubora wa chakula cha mifugo, hatua itakayoongeza tija kwa wafugaji.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deodatus Mwanyika, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kupongeza Taliri kwa kusimamia utekelezaji huo kwa ufanisi.
Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya mifugo ili kuhakikisha wafugaji wanapata mbegu bora za malisho na uhakika wa chakula cha mifugo.