

6 March 2025, 5:50 pm
Hospitali ya Taifa Muhimbili yenye kampasi mbili, ni Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini yenye vitanda 2,043 ambapo Upanga kuna vitanda 1,435 na Mloganzila vipo 608 ambapo Katika Kampasi zote mbili Wagonjwa 4,000 wanaonwa kwa siku.
Na Alfred Bulahya.
Imeelezwa kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na ya pili Kusini mwa Jangwa la Sahara kutumia, mtambo unaotumia tiba hewa yenye mgandamizo ya oksijeni kwa 100% (Hyperbaric Oxygen Therapy) ambao unatibu magonjwa zaidi ya 10.
Huu ni mtambo uliogharimu kiasi cha Tsh. milioni 250 katika ununuzi wake ambao umenunuliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Akiongea na waandishi wa habari marchi 6, 2025 Jijini Dodoma, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Prof.Mohamed Janab, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Hospitali ya Muhimbili,Upanga na Mloganzila,Dkt.Rechal Mhaville amesema kuwa hadi sasa wagonjwa 54 wamepona magonjwa mbalimbali ikiwemo vidonda sugu, na maumivu makali ya mgongo.
Aidha Dkt.Mhaville amesema Katika kipindi cha miaka minne iliyopita,hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma ya ubingwa bobezi wa kupima watoto wachanga kiwango cha kusikia mara tu wanapozaliwa ili kugundua mapema na kutoa matibabu ambapo tangu kuanzishwa huduma hiyo mwishoni mwa 2023 tayari watoto wachanga 320 wamenufaika na huduma hiyo.