Dodoma FM

MOI yafanikiwa kuanzisha huduma zaidi ya 10 za kibobezi

5 March 2025, 5:23 pm

Picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki akiongea na waandishi wa habari Jijini Dodoma . Picha na Alfred Bulahya.

Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 7 ya mwaka 1996 lengo likiwa ni kutoa huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

Na Alfred Bulahya.
Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), imefanikiwa kuanzisha huduma zaidi ya 10 za kibobezi ambazo hapo awali ziliwalazimu wagonjwa kuzifuata nje ya nchi.

Akizungumza March 5,2025 Jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisiya amezitaja huduma hizo.

Sauti ya Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisiya
Picha ni baadhi ya waandishi wa habari walio hudhuria mkutano huo.Picha na Alfred Bulahya.

Aidha ameutaja Muelekeo wa Taasisi hiyo akisema inajipanga Kuendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa ikiwa ni pamoja na kujenga benki ya mifupa.

Sauti ya Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisiya

Vile vile, Taasisi imeendelea kuwa hospitali ya kufundishia ya College of Surgeons of East, Central and Southern Africa (COSECSA) katika fani za ubobezi wa mifupa kwa watoto, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu na utoaji wa dawa za usingizi na ganzi tiba.

Kuhusu mipango ya baadae ya MOI ni kuendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao katika kiwanja cha MOI chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji jijini Dar es salaam.

Mpango mwingine ni kusogeza huduma katika jengo ambalo lilikua linatumika na Hospitali ya Tumaini Upanga ili sehemu ya wagonjwa wa nje waanze kupata huduma katika jengo hilo na kupunguza msongamano.

Aidha MOI inaendeleza jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi katika mikoa ambayo hajafikiwa ambayo ni Tanga, Ruvuma, Kigoma,Geita, Njombe, Manyara, Mara na Kagera.

Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 7 ya mwaka 1996 lengo likiwa ni kutoa huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, magonjwa ya ajali na kufanya tafiti kwenye maeneo haya na kufundisha wataalam na kupunguza ulemavu kwa wananchi.