

19 February 2025, 3:32 pm
Kwa mujibu wa taarifa ,Mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi huku Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma ikiendelea na kampeni ya usitishaji wa huduma ya maji kwa wateja ambao ni wadaiwa sugu.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) katika Operesheni ya ukusanyaji wa Madeni kwa wateja wenye Madeni Sugu na ukaguzi wa Miundombinu imebaini uwepo wa Mteja aliyechepusha maji (kuiba Maji) na kutumia katika kilimo cha zao haramu la Bangi.
Akithibitisha tukio hilo ,Meneja Ankara na Udhibiti wa madeni kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma DUWASA George Tito amesema walifanikiwa kupata taarifa za siri juu ya mteja huyo ambaye walimkatia maji kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Amesema mtuhumiwa huyu amekuwa akitumia maji hayo kwa shughuli za kilimo hasa kilimo cha Bangi ambapo tayari Jeshi la Polisi limechukua hatua juu ya mtuhumiwa huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Hamvu HALID MAJID amesema kitendo cha mwananchi huyo kuchepusha maji isivyo halali imesababisha baadhi ya maeneo ya mtaa huo kuwa na upungufu wa maji.
Ibrahim Mafita ni mkazi wa kata ya Chang’ombe amewasii wananchi wenzake kufuata utaratibu pindi wakiwa na madeni ili kujiepusha na uchepushaji wa maji.