

5 February 2025, 11:52 am
Amesema lengo la sensa hiyo ni kupata taarifa za kina za kitakwimu zitakazo iwezesha serikali na wadau kufanya maamuzi yenye ushahidi wa kitakwimu katika kuhuisha na kuboresha sera, mipango na program za maendeleo ya sekta ya viwanda na uchumi wa kitaifa kwa ujumla.
Na Mariam Kasawa.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Seleman Jafo amesema zoezi la Sensa ya uzalishaji Viwandani kwa Mwaka wa Rejea 2023 itafanyika mwezi March hadi June 2025.
Waziri Jafo ameyabainisha hayo Februari 4 wakati akizungumza na Vyombo vya Habari Jijini Dodoma kuhusu Sensa ya uzalishaji Viwandani kwa Mwaka wa Rejea 2023.
Aidha ametoa wito kwa wadau wote kuhakikisha wanashirikiana na serikali na kuhamasisha pamoja na kutoa elimu juu ya sensa hiyo.
Mhe. Dkt. Jafo amesema kuwa Sensa ya uzalishaji Viwandani ya mwaka wa Rejea 2023 itakuwa ya kwanza kufanyika katika pande zote mbili za Muungano wa Jamhuri ya Tanzania tangu mwaka 1964.
Aidha, suala la takwimu ni miongoni mwa mambo ya Muungano (namba 20 kwenye orodha ya mambo ya Muungano) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,Tanzania bara ilifanya Sensa za uzalishaji Viwandani mwaka 1963,1978,1989 na 2013 na Kwa upande wa Zanzibar zilifanyika mwaka 1989,2002,2008 na 2012.