Gari la wagonjwa kuondoa kero ya usafiri wa dharula Chifutuka
14 January 2025, 12:40 pm
Awali Wananchi wa Kijiji cha Chifutuka walilazimika kukodi magari binafsi na kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 90 hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ujio wa gari hilo umekuwa ahueni ya kupata tiba katika vituo na hospital za karibu.
Na Yussuph Hassan.
Wananchi wa kijiji cha Chifutuka Wilayani Bahi Mkoani Dodoma wamepongeza juhudi za serikali kwa kutatua changamoto ya gari ya kubebea wagonjwa iliyokuwa ikiwakabili wakazi hao.
Wameyabainisha hayo katika makabidhiano ya Gari hilo linalotarajiwa kuimarisha huduma za afya, hasa kusafirisha wagonjwa wa rufaa kwenda hospitali ya wilaya au Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Wamesema msaada huo utaondoa kero ya usafiri wa dharura, hasa kwa wanawake wajawazito na wagonjwa waliokuwa wakihitaji huduma za haraka.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo, amewataka wananchi wa Chifutuka kulitumia gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa pekee, akisisitiza umuhimu wa kuepuka matumizi yasiyo sahihi.
Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Chifutuka, Dk. Edson Luvakubusa, amesema gari hilo litasaidia kuboresha huduma za dharura na kuokoa maisha ya wagonjwa kwa urahisi zaidi.