PDPC yazikumbusha taasisi za umma na binafsi usajili ulimalizika disemba 31
10 January 2025, 5:38 pm
Uzingatizi si tu hitaji la kisheri bali pia ni kiashiria cha uwajibikaji wa taasisi na dhamira ya kulinda haki za wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 16(1).
Na Lilian Leopord.
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) inazikumbusha taasisi zote za umma na binafsi kwamba muda wa usajili wa hiari, kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulimalizika 31 Disemba 2024.
Akizungumza Mkurugenzi Mkuu- PDPC, Dr. Emmanuel Lameck Mkilia akiwa katika mkutano na waandishi wa Habari jijini Dodoma amesema kuwa bado kuna idadi kubwa ya taasisi ambazo hazijajisajili mpaka sasa.
Dr. Emmanuel ameongeza kuwa PDP imetoa fursa ya mwisho kwa taasisi ambazo hazijajisajili kabisa na ambazo hazijakamilisha usajili hadi kufikia tarehe 30 April, 2025. Pia, ameongeza kuwa taasisi zitakazoshindwa kujisajili ndani ya muda huo zitachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha ameongeza kuwa PDPC itaendelea kutoa elimu na miongozo kwa umma na kwa taasisi zinazofanya mchakato wa usajili na kuongeza uelewa kwa umma kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi.
PDPC inasisisitiza kwamba kulinda taarifa ni jukumu la kisheria na msingi wa ajenda ya mabadiliko ya kidigitali nchini.