Jamii yatakiwa kuwa na desturi ya kuwatembelea wagonjwa
2 January 2025, 5:39 pm
Wadau mbalimbali wameombwa kufika katika hospitali mbalimbali ili kujua changamoto zinazowakabili wagonjwa.
Na Seleman Kodima.
Wito umetolewa kwa jamii kuwa na desturi ya kuwatembelea wagonjwa na kuthamini jumuiya zinazojitolea kuhudumia wagonjwa katika Hospitali mbalimbali hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ambaye ni Afisa Tarafa Dodoma mjini Bi Zainabu Issa alipotembelea wagonjwa na kuwalisha vyakula kwa kushirikiana na marafiki wa Shekimweri katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza baaada ya zoezi hilo Bi Zainabu amewaomba wadau wengine kufika katika hospitali mbalimbali ili kujua changamoto zinazowakabili wagonjwa.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, kupitia mwakilishi wake Paul Mageni amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Dodoma pamoja na Marafiki zake kwa tukio hilo na kuziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi inayojihusisha na kutoa huduma kwa wagonjwa na yatima Jai mkoa wa Dodoma Ally Kanda amesema kitendo cha taasisi hiyo kushirikishwa katika zoezi hilo ni ishara ya kutambua mchango wao.
Malick Masoud na Khadija Yussuph ni Marafiki wa Shekimweri wameeleza mguso wa tukio hilo ambalo wamelifanywa kwa ajili ya kuwa sehemu ya jai katika kuhudumia wagonjwa.