Dodoma FM

RC Dodoma kufungua tamasha la 7 la jinsia wilaya ya Kondoa

26 August 2024, 7:10 pm

Picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi akiongea na waandishi wa habari kuhusu tamasha hilo.Picha na Mariam Kasawa.

Na Mariam Kasawa.

Zaidi ya Wanaharakati na Wadau 300 wanaotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia kutoka pande mbalimbali nchini wanatarajia kushiriki katika Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa., Mkoani Dodoma.

 Akitoa Tamko leo Jumatatu Agosti 26,2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi amesema Tamasha hilo la siku tatu litakaloongozwa na mada kuu ‘Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange’ linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule.

Amesema Tamasha la 7 la Jinsia ngazi ya Wilaya limeandaliwa na TGNP kwa kushirikiana na mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia nchini wakiwemo WFT, CAMFED, WAJIBU, Chuo cha  Mafunzo ya Serikali za Mitaa, Policy Forum, PELUM Tanzania,  na Msichana Initiative,  Vituo vya Taarifa na Maarifa kutoka Mtwara Vijijini, Lindi, Same, Mwanga, Babati, Morogoro Vijijini, Gairo, Kinondoni, Ilala, Ubungo, Kondoa Vijijini na Kishapu.

Liundi ameeleza kuwa, wameandaa tamasha hilo kwa ufadhili wa wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Ubalozi wa Uswidi, CrossRoads International UN Women, Coady international, Ubalozi wa Ireland, Global Affairs Canada kupitia Seedchange na Aga Khan Foundation.

Hali kadhalika kutafanyika Maonesho katika siku zote za Tamasha kutoa nafasi kwa mashirika na mitandao inayoshiriki kuonesha kazi zao kupitia njia mbalimbali kama vile video, mabango, picha ambapo Wachapishaji, AZAKI na wanawake binafsi pia wanakaribishwa kuonesha na kuuza bidhaa zao na kwamba sehemu maalumu zitatolewa kwa vikundi maalum kutengeneza vitovu vya mtandao, kupeana taarifa na kupanga mikakati ya pamoja. 

Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 litaongozwa na mada kuu isemayo ‘Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange’  huku mada ndogo ndogo zikiwa ni pamoja na  Miaka 30 baada ya Beijing: Viongozi wanawake wako wapi? Mada hii itajikita kuangazia namna yakuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi hasa kwenye nafazi za viongozi wa serikali za mitaa kuelekea uchaguzi wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025 wa Madiwani, Wabunge na Rais.