Dodoma FM

Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA watakiwa kufanya kazi kwa uadilifu

21 August 2024, 6:25 pm

Picha ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko akizungumza katika hafla ya Utiaji Saini Mikataba ya utekelezaji wa Miradi wa Kupeleka Umeme katika vitongoji 3,060 (15 kila Jimbo) jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Nishati.

Vitongoji takribani 3,060 vitapatiwa umeme kupitia mradi huu kwa gharama ya Jumla ya bilioni 366.

Na Pius Jayunga

Wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya Kimkakati ya Nishati hususan Miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kukamilisha kwa wakati na REA kuwasimamia Wakandarasi kwa kutenda haki.

Hayo yamebaibishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko wakati wa hafla ya Utiaji Saini Mikataba ya utekelezaji wa Miradi wa Kupeleka Umeme katika Vitongoji 3,060 (15 kila Jimbo) Jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa, mpango wa kupeleka Umeme kwenye Vitongoji utatekelezwa kwa awamu huku akisisitiza uwajibikaji wa dhati kwa REA na Wakandarasi hao.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Said,  amesema matarajio yaliyopo sasa ifikapo mwezi Septemba 2024 ni kuhakikisha wanafikisha Umeme kila sehemu hapa Nchini.