Dodoma FM

Serikali kuhakikisha zabibu inapata soko la uhakika

20 August 2024, 5:17 pm

Picha ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango wakati akizungumza na wananchi katika ziara yake mkoani Dodoma.Picha na Wizara ya Kilimo.

Kiwanda hicho kimegharimu kiasi cha Shilingi Billioni 2.1 na kinauwezo wa kusindika tani 7-8 kwa siku ambapo sawa na kuhifadhi lita 1500 za mvinyo.

Na Fred Cheti

Upatikanaji wa soko la uhakika wa zao la zabibu mkoani Dodoma unatarajia  kuongeza tija na chachu kwa wakulima wa zao hilo kutokana na jitihada zinazoendelea kufanywa katika kuimarisha uzalishaji wa zao hilo.

Hii ni baada ya kauli ya serikali kupitia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango kuwataka wananchi kuongeza uzalishaji wa zao la zabibu na mengine ya kimkakati kwa sababu ardhi ya Dodoma ni rafiki kwa kilimo hivyo serikali imejipanga katika upatikanaji wa masoko ya uhakika ya zao la zabibu kutokana na kuongezeka kwa wanywaji wa mvinyo.

Mara kadhaa Wakulima wengi Mkoani hapa wamekuwa wakilalamika suala la Masoko ya uhakika wa zao hilo ambalo linatajwa kama miongoni mwa mazao ya kimkakati Mkoani Dodoma hivyo kupatikana kwa Masoko hayo ya uhakika kutaleta ahueni kwao.

Agosti 19 mwaka huu akizindua Kiwanda cha kusindika Zabibu kilichopo Chinangali II, Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma katika ziara yake ya Kikazi Mkoani hapa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alisema lengo la Serikali ni kuongeza upatikaniji wa Masoko ya uhakika ya zao hilo.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema mbali na Kiwanda cha usindikaji wa Zabibu Serikali itaendelea kuweka Mazingira rafiki kwa Wakulima wa zao hilo ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi.

Tanzania hutumia takriban Shilingi Bilioni 19.5 kila mwaka kuagiza wastani wa Lita Milioni 10 za Mchuzi wa Zabibu nje ya Nchi ili kukidhi mahitaji ya ndani. Hivyo, Kiwanda hicho kinakwenda kusaidia usindikaji na uhifadhi wa Zabibu na kuzuia upotevu wa mavuno ambao awali ulichangiwa na kukosekana kwa miundombinu ya kuongezea thamani ya zao hilo.