DC Kongwa: Simamieni lishe kuzuia utapiamlo
14 August 2024, 5:46 pm
Fedha zilizopangwa kutumika katika kutekeleza afua za lishe ni shilingi 27,183,940.14 sawa na asilimia 91.83 ya fedha zilizotumika kwa ajili ya chakula shuleni na kutekeleza siku ya afya ya lishe vijijini ambapo vijiji 87 na mitaa 28 vilishiriki kikamilifu .
Na Bernadetha Mwakilabi.
Mkuu wa Wilaya Kongwa Mh.Mayeka Saimon Mayeka amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kusimamia upandaji wa miti ya matunda katika taasisi zote, ofisi za watendaji wa vijiji na kata uwepo wa vyoo vizuri vinavyotumika katika kila kaya .
Mayeka ameyasema hayo jana katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2023/24 uliojumuisha wadau mbalimbali wa Lishe ambapo Kata za Matongoro, Sagara na Mamlaka ya mji mdogo Kongwa, hospital ya wilaya Kongwa, kituo cha afya Mlali na Ugogoni na mdau kutoka shirika la CUAMM doctors with Africa walipatiwa hati za ushindi wa utekelezaji mkaba huo kwa mwaka 2023/2024.
Aidha Mayeka amepiga marufuku mikokoteni inayokokotwa na Ng’ombe kutembea barabarani zaidi ya saa moja kamili jioni kinyume na hapo wakamatwe na kuchukuliwa hatua ili kuwa na usalama barabarani.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kongwa Dr Omary Nkullo amewataka maafisa ustawi wa jamii kuongeza nguvu ya ushawishi katika kutoa elimu kwa jamii juu ya masuala ya lishe ili kuepukana na suala la utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ndani ya wilaya ya hiyo.
Kwa upande wake Afisa lishe wilaya ya Kongwa Bi Maria Haule ameeleza kuwa katika kupambana na utapiamlo wilaya hiyo imefanikiwa kununua mashine nne za kuongeza virutubishi shuleni, kuongeza idadi ya wanafunzi wanaokula chakula kwa kipindi cha Januari hadi machi kutoka wanafunzi 99,009 hadi 126,936 .