Wananchi wahitaji elimu zaidi ugonjwa wa homa ya ini
31 July 2024, 7:17 pm
Kwa mujibu wa wataalam wa afya wanabainisha njia za maambukizi ya homa ya Ini zinashabihiana sana na zile za maambikizi ya Virusi Vya Ukimwi.
Na Witness.
Ikiwa kila ifikapo Julai 28 dunia huadhimisha Siku ya Homa ya Ini Duniani, takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2021 zinaonesha duniani kati ya watu wapatao milioni 296 ambao wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina B na watu milioni 58 wanaishi na maambukizi sugu ya Virusi vya Homa ya Ini aina C.
Hii ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya ambapo hivi karibuni Tanzania iliadhimisha siku hiyo ikienda sambamba na kauli mbiu isemayo “Ni wakati wa kuchukua hatua”
Kwa kufahamu jamii ina uelewa kiasi gani juu ya ugonjwa wa homa ya ini, Taswira ya Habari imezungumza na wakazi jijini Dodoma na hapa wanabainisha uelewa wao.
Pamoja na hayo wameomba Elimu itolewa zaidi ya juu maambukizi ya ugonjwa wa homa ya Ini.
Hivi karibuni Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini, Eva Uiso kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga wakati akitoa Elimu kwa Jamii amesema kuwa inakadiriwa kuwa Duniani kote zaidi ya Watu Milioni 250 wanaishi na virusi vya ugonjwa wa homa ya Ini (Hepatitis B) ambapo kiasi kikubwa cha Watu walioambukizwa wako Bara la Afrika na Ulaya.
Kwa mujibu wa Wataalam wa Afya wanabainisha njia za maambukizi ya homa ya Ini zinashabihiana sana na zile za maambikizi ya Virusi vya Ukimwi, njia hizo kuwa ni kuongezewa damu ya Mtu mwenye maambukizi ya Virusi vya homa ya Ini, kujichoma na vitu vyenye ncha kali kama vile kutumia Sindano hususani kwa wale wanaotumia dawa za kulevya, ngono zisizo salama na maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto wakati wa kujifungua.