Umeme wa REA waimarisha huduma za afya Hombolo Bwawani
29 July 2024, 7:53 pm
Mikoa mingine inayotekelezwa na mradi huo ni Mwanza, Kagera, Simiyu, Arusha, Pwani, Lindi na Mtwara.
Na Mindi Joseph.
Baadhi ya Wananchi kutoka katika Mitaa ya Kolimba na Hombolo Bwawani Kata ya Hombolo Jijini Dodoma wamesema uwepo wa huduma ya Umeme wa kupitia (REA) umekuwa na Mchango mkubwa katika uboreshaji wa huduma za Afya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Dodoma Tv baadhi ya Wananchi kutoka Kata ya Hombolo Mkoani Dodoma wamesema Umeme wa REA umekuwa na tija kubwa katika maeneo yao hasa kwenye Sekta ya Afya.
Hii ni baada ya Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) katika kutekeleza Mradi wa kupambana na Magonjwa ya Mlipuko ikiwemo Kipindupindu na Uviko-19 kusambaza Umeme katika visima ambavyo havikuwa na pampu za Umeme za kuvuta maji na vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mkoa wa Dodoma kwa Wilaya za Dodoma, Chamwino, Bahi, Chemba, Kongwa na Mpwapwa.
Kwa mujibu wa REA hadi kufikia Mwezi Julai, 2024, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeunganisha Umeme katika Vijiji 12,167 kati ya Vijiji 12,318 ambayo ni sawa na 98.8% ya Vijiji vyote vya Tanzania Bara na hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2024 Vijiji vyote 12,318 vitakuwa vimeunganishwa na huduma ya Umeme Tanzania Bara sawa na asilimia 100.