DUWASA yaendelea kutekeleza azma ya kuifanya Dodoma ya kijani
18 March 2024, 5:34 pm
Utekelezaji wa zoezi hilo unabeba dhana ya kuhakikisha maeneo ya vyanzo vya maji yanakuwa salama katika athari za mabadiliko ya tabianchi.
Na Mariam Kasawa.
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Alhaji Jabiri Shekimweri ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kutekeleza kwa vitendo azma ya kukijanisha Dodoma kwa upandaji wa miti katika eneo la Tanki kubwa la maji Nzuguni.
Pongezi hizo amezitoa wakati wa zoezi la upandaji wa miti 300 kwenye eneo la Tanki kikubwa la maji linalopatikana Nzuguni.
Alhaji Jabiri Shekimweri amesema kuwa kitendo cha mamlaka hiyo kutii agizo lake la kupanda miti yenye kimo cha wastani kitawezesha miti hiyo kukua bila changamoto yeyote ya kimazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema kuwa kuanzia Novemba mwaka jana hadi leo jumla ya miti 2000 imepandwa katika maeneo tofauti ya vyanzo vya maji ikiwa ni utekelezaji na utunzaji wa vyanzo hivyo.