Wafanyabiashara wa Mchele Bahi walia kukosa soko la uhakika
24 January 2024, 11:55 pm
Mamlaka zinazohusika na suala hili zinatakiwa kuharakkisha upatikanaji wa huduma ya soko ili wakulima wa mpunga waweze kuuza mchele badala ya kuuza mpunga ambao wanaeleza kuwa faida yake ni ndogo.
Na Bernad Magawa.
kukosekana kwa soko la uhakika la mchele wilayani Bahi imeelezwa kuwa ni moja ya sababu inayorudisha nyuma maendeleo ya wakulima wa mpunga huku wafanyabiashara wa mchele wakilalamikia ugumu katika kutafuta masoko ya mchele ambao unazalishwa kwa wingi wilayani Bahi.
Wanasema licha ya wilaya ya Bahi kuzalisha kwa wingi mpunga kwenye ukanda huu wa kati, lakini bado ukifika wilayani hapa kwa mara ya kwanza huwezi kuona kwa haraka kiashiria chochote cha uwepo wa zao hili kwa wingi kwani hakuna soko rasmi kwa ajili ya kuuza na kununua mchele, isipokuwa ni kwenye mashine za kukoboa mpunga ndipo walipojishikiza wafanyabiashara wa mchele.
Hali hii ya kukosekana kwa soko wilayani hapa inasababisha mchele kuuzwa kwa bei kubwa kama vile haulimwi hapa kwani wafanyabiashara wengi wamekuwa wakinunua mpunga na kuusafirisha maeneo mengine badala ya kuukoboa na kuuza mchele hapa hali inayopelekea vijana wengi wanaojishughulisha na uuzaji wa mchele kukosa fursa.
Pamoja juhudi za muda mrefu za serikali kuweka soko wilayani hapa lakini bado juhudi hizo hazijazaa matunda hali inayopelekea wajasiliamali wakiwemo akina mama kuendelea kupaza zauti.