Maafisa ustawi jamii watakiwa kutoa elimu ya afya ya akili
7 September 2023, 1:00 pm
Mkutano wa Maafisa ustawi wa jamii umefunguliwa jana jijini Dodoma ambao utadumu kwa muda wa siku mbili na kuwakutanisha maafisa ustawi wa jamii Nchi nzima ili kujadili namna ya kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi.
Na Yussuph Hassan.
Maafisa ustawi wa jamii Nchini wametakiwa kutoa Elimu ya Afya ya akili na msaada wa Kisaikolojia kwa jamii ili kupunguza na kumaliza vitendo vya ukatili.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha maafisa ustawi wa jamii Jijini Dodoma Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko ametoa maagizo kwa Maafisa ustawi wa jamii huku akisema kuwa changamoto ya afya ya akili huchangia vitendo vya ukatili.
Aidha amewataka Wazazi na Walezi kusimamia kikamilifu malezi ya Watoto kwani kusambaratika kwa familia ni moja kati ya sababu za kuwepo kwa wimbi la watoto wa mtaani.
kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dkt .Dorothy Gwajima amesema kuwa Maafisa ustawi wa jamii wamekuwa na msaada mkubwa Nchini kupitia nyanja mbalimbali.