Wananchi watakiwa kujitokeza kuonesha bidhaa zao maonesho ya 88
31 July 2023, 6:11 pm
Sherehe za maonesho ya nanenane hufanyika kila mwaka ifikapo Augost 8, ambapo kauli mbinu ya mwaka huu kitaifa ni, vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula, huku kauli mbiu ya kikanda ikisema kilimo ni biashara na biashara ni uwekezaji.
Na Alfred Bulahya.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule amewataka wananchi wa maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya Kati, kujitokeza kwa wingi kuonesha bidhaa zao katika sherehe za maonyesho ya 88 mwaka 2023, zinazotarajia kuanza mapema kesho jijini hapa.
Ametoa rai hiyo mapema leo ofisini kwake wakati akitoa tamko rasmi mbele ya waandishi wa habari, la kuanza kwa sherehe hizo hapo kesho ambazo zitahusisha mikoa ya Dodoma na Singida.
Mh. Senyamule amesema sherehe za maonesho ya mwaka huu zimelenga kuongeza hamasa ya kuzalisha mazao ya chakula na mifugo kwa tija, kupitia teknolojia mbalimbali zitakazooneshwa.
Mbali na hayo amesema katika maonesho hayo wanatarajia kuwaalika wataalamu na wabobezi wa masuala ya kilimo na ufugaji ili kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji.
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Machinga Complex lililopo jijini hapa wameeleza walivyojipanga kushiriki na namna gani watanufaika na sherehe za maonesho hayo.