Serikali kuwashughulikia waajiri sugu wanaodaiwa michango ya wafanyakazi
21 June 2023, 4:21 pm
Serikali imeanzisha mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kulipa mafao ya mtumishi pindi mfanyakazi anapostaafu au kuacha kazi.
Na Mindi Joseph.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameagiza wakurugenzi wakuu wa PSSSF na NSSF kuhakikisha kila meneja wa Mkoa anawasilisha majina ya waajiri Sugu wanaodaiwa michango ya wafanyakazi ndani ya siku 7.
Akizungumza leo jijini Dodoma na waandishi wa habari Mhe. Katambi amesema pamekuwepo na changamoto kwa baadhi ya waajiri kutowasilisha michango au kuwasilisha michango pungufu ya watumishi wao.
Mh Katambi ametaka waajiri wote kuhakikisha wanalipa na kuwasilisha madeni ya michango ya watumishi wao kila mwezi.
Katika hatua nyingine amesema kutowasilishwa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ni kosa kisheria.
Juni 19 mwaka huu katika bunge la 12 mkutano wa kumi na moja kikao cha hamsin Spika wa Bunge dkt. Tulia Ackson aliiagiza ofisi ya waziri mkuu kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu kuisimamia mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo NSSSF pamoja na PSSSF kuwabana waajiri ambao hawawasilishi michango ya wafanyakzi wao kwa wakati.