Asilimia 97 watumiaji dawa wamefanikiwa kufubaza virusi vya Ukimwi
14 June 2023, 3:24 pm
Waziri Ummy ametoa wito kwa Watanzania kwenda kupima kujua hali zao lakini kwa ambao wanajua hali zao dawa za UKIMWI zipo na zinatolewa bila malipo na vipimo vya kujipima mwenyewe vipo kwahiyo Watanzania wajitokeze kupima ili tutokomeze UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Na Fred Cheti.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha kuwa katika kila watu 100 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi watu 86 wanajitambua kuwa wana maambukizi ya UKIMWI ambao ni sawa na 86% huku wanaotumia dawa wakiwa ni 97% kwa Tanzania.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati alipotembelea kituo cha afya Makole akiambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Angela Kairuki pamoja na ugeni kutoka mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Ukimwi US-PEPFAR, Global Fund na UNAIDS Jijini Dodoma.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa katika kila watu 100 Tanzania wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na wanaojua hali zao ni asilimia 97 ambao wanatumia dawa na wamefanikiwa kufubaza virusi hivyo kwa kujiepusha na maambukizi ya magonjwa mengine na wanaweza wasiwaambukize watu wengine.
Kufuatia hali hiyo Dodoma Tv Imezungumza na baadhi yawananchi jijini hapa kuhoji je kwa sasa jamii inamwamko wa kutosha juu ya kupima na kujua hali zao?