Mbunge wa jimbo la Bahi atoa millioni 16 ujenzi wa Zahanati ya Mapinduzi Kigwe
11 May 2023, 4:26 pm
Amesema zahanati hiyo itawaondolea adha wananchi hao ya kufuata huduma za afya kituo cha afya kigwe.
Na Bernad Magawa.
Mbunge wa jimbo la Bahi Mheshimiwa Kenneth Nollo ametoa Millioni 16 kujenga zahanati ya kijiji cha Mapinduzi kata ya kigwe ikiwa ni kuendelea kutekeleza mkakati wake wa kuhakikisha vijiji vyote vya jimbo la Bahi vinakuwa na kituo cha kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Nollo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mapinduzi kwenye mkutano wa hadhara alioufanya kijijini hapo alipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho amesema zahanati hiyo itawaondolea adha wananchi hao ya kufuata huduma za afya kituo cha afya kigwe, na baadaye akajumuika na wananchi katika kazi ya kumwaga zege kwaajili ya kuweka jamvi la jengo hilo.
Nollo amesema zahanati hiyo ni ya 13 tangu aingie katika nafasi hiyo mwaka 2020 na kuongeza kuwa tayari zahanati 12 zipo katika hatua ya umaliziaji na Muda wowote zitaanza kutoa huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Nollo amewashukuru wananchi wa kijiji cha Mapinduzi kujitokeza kwa wingi katika kazi ya kumwaga jamvi la jengo hilo la zahanati na kuwahamasisha kuendelea kushikamana katika kazi za maendeleo kijijini hapo.
Baadha ya hotuba ya Mheshimiwa Nollo, wananchi walijawa na furaha, hatimaye burudani zikatawala kumpongeza kiongozi huyo.