Wananchi kibaigwa wafunguka kero wanazo pata katika huduma za jamii
3 May 2023, 5:11 pm
Shilingi milioni 150 imetengwa kwaajili ya kuongeza vifaa tiba ambapo kabla ya kufika mwezi wa Saba mwaka huu kituo cha afya kibaigwa kitaanza kutoa huduma za upasuaji.
NA, Bernadetha Mwakilabi.
Wakazi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa ulioko wilayani Kongwa wameiomba Serikali kushughulikia kero zinazowakabili katika nyanja mbalimbali za kijamii.
Wakitoa kero hizo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa wananchi hao wameiomba serikali kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma za Jamii kwenye Sekta za Elimu, Afya, Maji, barabara, umeme, Ardhi na Mazingira.
Miongoni mwa wananchi hao Bwana Yohana Makavu aliyehoji sababu za kituo cha Afya Kibaigwa kushindwa kutoa dawa kwa wateja wa bima za Afya, na kuwataka kuzinunua katika katika duka la kituo Cha afya.
Akijibu hoja hiyo kwa niaba ya Mganga Mkuu (W), Katibu wa Afya Abdallah Missenye amesema Serikali imeruhusu kuwepo kwa maduka ya dawa ya Jamii ili kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa, jibu ambalo wananchi hawakuliafiki.
Pia Missenye amesema Shilingi milioni 150 imetengwa kwaajili ya kuongeza vifaa tiba ambapo kabla ya kufika mwezi wa Saba mwaka huu kituo cha afya kibaigwa kitaanza kutoa huduma za upasuaji.
Licha ya kuahidi kutatua kero hizo mkuu wa wilayani Kongwa Mh. Remidius Mwema Emmanuel amewataka wananchi kuzingatia sheria katika utekelezaji wa shughuli zao ikiwa ni pamoja na kutojihusisha na biashara za magendo kwa kuwa Serikali haitomfumbia macho mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara haramu zikiwemo dawa za kulevya
Sambamba na hayo Mwema ameiasa Jamii kuzingatia Maadili ili kuwalea watoto katika Mazingira wezeshi kielimu.