Wananchi washiriki ujenzi wa barabara Bahi sokoni
27 March 2023, 3:42 pm
Na Bernad Magawa.
Wananchi wa kijiji cha Bahi sokoni wamejitokeza kwa wingi kushiriki Ujenzi wa Barabara inayotarajiwa kuunganisha mawasiliano ya wananchi wa kijiji hicho na kitongoji cha Sanduli ambacho hakikuwa na barabara.
Barabara hiyo ambayo inajengwa kwa nguvu za wananchi kama ajira za muda kupitia mradi wa walengwa wa Tasaf imeeleza kuwa mkombozi kwa wananchi wa kitongoji hicho huku ikifungua mawasiliano ya karibu kati ya kijiji cha Bahi sokoni kuelekea kilipojengwa chuo cha veta wilaya ya Bahi.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Bahi sokoni Regnado Ndahani amesema wananchi wamejitokeza kwa wingi kushiriki mradi huo na kueleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kitongoji cha sanduli.
Nao baadhi ya wananchi wanaoshiriki kujenga barabara hiyo wameeleza kwa furaha namna wanavyonufaika na mradi huo huku wakielekeza shukrani zao kwa serikali kwa kuwapelekea mradi ambao unawawezesha wao kujipatia kipato.
Mradi huo wa ajira za muda kwa wanufaika wa Tasaf unalenga kunufaisha zaidi ya wananchi 250 ambao wanatarajia kujenga barabara yenye zaidi ya kilomita 6 kutoka kijiji cha bahi sokoni hadi kitongoji cha sanduli ambacho ni sehemu ya vitongoji vya kijiji hicho ambacho hakikuwahi kuwa na mawasiliano ya barabara.