Kanisa la Pentekoste Mtakuja lamtaka Mkuu wa wilaya kutatua mgogoro wa ardhi
27 March 2023, 3:10 pm
Huu ni Muendelezo wa kanisa hilo katika harakati za kuomba serikali ya wilaya ,mkoa na wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweza kumaliza mgogoro huo ambao wameshindwa kujua ni lini utapata ufumbuzi.
Na Seleman Kodima.
Uongozi wa kanisa la Pentekoste christian International linalopatikana mtaa wa Mtakuja kata ya Chang’ombe limesema halijaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na idara ya ardhi baada ya serikali ya wilaya kufika eneo hilo kushuhudia kinachoendelea kupitia mgogoro wa ardhi .
Hili linajiri baada ya kanisa hilo kumuandikia barua mkuu wa wilaya ya Dodoma Mhe Jabiri Shekimweri mapema Mwezi huu wakimuomba aweze kufika eneo hilo ili kuwasaidia kutatua mgogoro wa ardhi kati ya kanisa hilo na mwanajamii ambaye anadaiwa kumega eneo katika kanisa hilo.
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya alimtuma mwakilishi ambaye ni afisa taarfa wa Dodoma ambaye aliweza kutoa ahadi juu ya maamuzi yatakayotolewa wiki mmoja baade ambapo watalaamu wa upimaji wa ardhi kutoka halmashauri ya jiji walifanya urejeo na uhakiki wa ramani ya upimaji uliofanyika .
Mapema jana Askofu wa kanisa hilo Thomas Kiula amekiri kupokea barua kutoka halmashauri ya jiji la Dodoma ambapo amesema bado ombi lao mahususi halijatatuliwa na kumuomba Mkuu wa wilaya ya Dodoma kufika mwenyewe ili aweze kutoa haki ambayo ni msingi wa mgogoro huo wa ardhi.
Nao baadhi ya Wanakamati wa kikosi kazi ya upimaji wa ardhi mtaa wa mtakuja ambao walihusika awamu ya kwanza ya upimaji wa eneo hilo wameiomba serikali kufika eneo hilo ili kutatua mgogoro ambao umeanza kuleta taswira mbaya serikali ya mitaa na wanajamii
Kwa upande wa waumini wa kanisa hilo wakizungumza na Taswira ya Habari wametoa masikitiko yao juu ya kile kinachondelea kuhusu kumegwa kwa eneo la kanisa hilo ambapo kiasili lilikuwa ni eneo lenye kutambuliwa kuwa ni sehemu ya kanisa hilo ,hata upimaji wa ardhi awamu ya kwanza ulianisha hivyo.
Huu ni Muendelezo wa kanisa hilo katika harakati za kuomba serikali ya wilaya ,mkoa na wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweza kumaliza mgogoro huo ambao umekosa kujua ni lini utapata ufumbuzi ili hali baadhi ya Viongozi wamekuwa wakitoa maamuzi yenya kushindwa kuleta suluhu baina ya kanisa na wanajamii na serikali ya mtaa huo.