DC Gondwe apiga marufuku wanafunzi kuchunga mifugo siku za masomo
16 March 2023, 3:39 pm
ni vema wazazi kupunguza tabia ya kuwa wakali kwa watoto wao na badala yake wajenge urafiki kwa kuzungumza nao mara kwa mara ili wasiwaogope , bali wawe huru kwa wazazi wao kueleza changamoto mbalimbali.
Na Benard Magawa
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe amepiga marufuku watoto wote wenye umri wa kwenda shule kuchunga mifugo siku za masomo na kuagiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shuleni kila siku ili wapate elimu itakayowasaidia watakapokuwa watu wazima.
Mheshimiwa Gondwe ameyasema hayo mapema wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bahi sokoni kwa lenga kusikiliza kero za wanachi.
Gondwe amewaomba wazazi, walezi, wiongozi wa dini, viongozi wa Serikali, na wazee wilayani humo kushirikiana katika kuhimiza na kusimamia suala la elimu, kwani serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya elimu hivyo ni vema watoto wote wa Tanzania wakanufaika na fursa ya elimu bure bila kuikosa.
Aidha amewahimiza wazazi na walezi kuwalea watoto wao katika maadili bora huku akisisitiza kuhakikisha wanapambana na suala la ukatili wa kijinsia kwa watoto na akina mama ili kuwa na kizazi bora chenye maadili.
Amesema ni vema wazazi kupunguza tabia ya kuwa wakali kwa watoto wao na badala yake wajenge urafiki kwa kuzungumza nao mara kwa mara ili wasiwaogope , bali wawe huru kwa wazazi wao kueleza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kuhusu ukatili wa kijinsia katika jamii.
Amehimiza jamii ya wana Bahi kupiga vita ukatili wa kijinsia kwani unawaharibu watoto wengi kisaikolojia na kujikuta wanashindwa kutimiza malengo yao katika masomo, amewasihi wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa kwa vyombo vya sheria kuhusu matukio yote ya ukatili wa kijinsia ili yaweze kuchukuliwa hatua kwa za haraka.