Wananchi watarajia kuondokana na tatizo la kukosekana kwa daraja Bahi
15 March 2023, 3:23 pm
Wananchi wanatarajia kuondokana na tatizo la kukosekana kwa daraja la Mto Nkogwa kutokana na daraja lililokuwepo hapo awali kusombwa na maji mwisho mwa mwaka jana.
Na Bernad Magawa.
Wananchi wa kijiji cha Bahi sokoni wilaya ya Bahi Wanatarajia kuondokana na tatizo la kukosekana kwa daraja la Mto Nkogwa kutokana na daraja lililokuwepo hapo awali kusombwa na maji mwisho mwa mwaka jana.
Daraja hilo ambalo linaunganisha wananchi wanaoishi vitongoji vilivyopo upande wa pili wa kijiji cha Bahi sokoni na yalipo makao makuu ya wilaya ya Bahi limekuwa kero kwa wananchi pindi maji yanapojaa huku watumiaji wa magari wakilazimika kuzunguka umbali mrefu ili kufika Bahi sokoni.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bahi sokoni Diwani wa kata ya Bahi Mheshimiwa Agostino Ndonu amesema tayari serikali imetenga fedha kwa mwaka 2023/2024 kujenga barabara inayokwenda Bahi sokoni kwa kiwango cha lami pamoja na kujenga daraja kubwa katika mto nkogwa.
Awali akieleza kuhusiana na changamoto hiyo Michael Mlelwa, mkazi wa kijiji cha Bahi Sokoni amesema kuharibika kwa miundombinu hiyo kumeleta adha kubwa kwa wananchi na kuiomba serikali kuharakisha ujenzi huo.
Kwa mujibu wa wananchi wanaoishi katika kitongoji cha miembeni kijiji cha Bahi sokoni, wamesema kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakisumbuliwa na maji kujaa katika makazi pindi mto Nkogwa unapofurika na kuharibu baadhi ya mali zao.
Kujengwa kwa daraja na barabara hiyo kutaondolea adha kubwa wakulima wa Mpunga wilayani Bahi ambao wengi hutegemea barabara hiyo kwaajili ya kurudisha mazao yao kutoka mashambani pamoja na wananchi wanaokwenda kupata huduma za afya kituo cha afya Bahi.