Watendaji wa kata Bahi waishukuru Serikali
1 March 2023, 4:00 pm
Hapo awali watendaji hao walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri hasa katika kuzungukia kata zao lakini kwa sasa wanaweza kufuatilia mianya yote ya upotevu wa mapato kwa kutumia pikipiki walizopewa kuhakikisha wanakuza pato la halmashauri na serikali kwa ujumla.
Na. Benard Magawa
Baadhi ya watendaji wa kata wilayani Bahi mkoani Dodoma wameishukuru Serikali kuwapatia vyombo vya usafiri kwa ajili ya kuwasaidia katika kusimamia ulinzi na usalama kwenye kata zao na kuwarahisishia ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Wakizungumza na kituo hiki leo March 1, 2023 wamesema vyombo hivyo vya usafiri vitawasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti upotevu wa mapato ambayo mwanzo yalitoroshwa kwenye kata wanazofanyia kazi huku wakiahidi kutumia vyombo hivyo kwa umakini ili viweze kutimiza malengo tarajiwa kwa Serikali.
Nguluchila Paschal Mangwela Mtendaji wa kata ya Lamaiti, anaeleza namna Pikipiki aliyopewa itakavyo msaidia katika utendaji kazi wake ambao hapo mwanzo ilikuwa vigumu kuwajibika ipasavyo kutokana na eneo kubwa analolitumikia.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutuona na sisi watendaji wa kata, vyombo hivi vitatusaidia katika kudhibiti, kusimamia na kukuza ukusanyaji wa mapato ya serikali katika maeneo tunayofanyia kazi.”
Naye Afisa mtendaji wa kata ya Chikola Tatu Mshani amesema kupatikana kwa usafiri wa Pikipiki kutamuepushia gharama nyingi alizozitumia hapo awali kukodi usafiri kwaajili ya kufuatilia Mapato ya Serikali katika kata yake.
“Katika kata ya Chikola kuna uvuvi wa samaki hivyo samaki wanatolewa wakati wote, hapo mwanzo ilikuwa vigumu kufukuzia wafanya biashara wanaotoroka na ushuru kwa wakati kwani ilinilazimu kukodi pikipiki lakini kwa sasa mimi na migambo wangu tutafika kila mahali kwa wakati.” Amesema Mshama.
Wamesema hapo awali walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri katika kata zao lakini kwa sasa wanaweza kufuatilia mianya yote ya upotevu wa mapato kwa kutumia pikipiki walizopewa kuhakikisha wanakuza pato la halmashauri na serikali kwa ujumla.
Akikabidhi pikipiki 6 zilizotolewa na Serikali kwa lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa shughuli za ulinzi na usalama kwa watendeji sita wa kata wilayani Bahi mapema wiki iliyopita, Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe aliwaasa watendaji hao kuepuka matumizi mabaya ya vyombo hivyo na kuwaagiza kuvitumia kwaajili ya kazi za serikali.