Wakristo itumieni kwaresma kujipatanisha na Mungu
23 February 2023, 3:44 pm
Lazima tufanye mazoezi ya kiroho kwa kutubu kidogo kidogo na hatimaye tuweze kuacha dhambi kabisa, tusikubali kurudia katika dhambi.
Na Bernad Magawa
Wito umetolewa kwa wakristo kukitumia vizuri kipindi cha kwaresma kuwa kipindi cha kufanya toba, kujipatanisha kiroho na kumrudia Mungu kwa kuacha matendo maovu, kujinyima na kuwasaidia wahitaji kadiri ya miongozo ya dini.
Hayo yamesemwa na Paroko wa Parokia ya Bahi iliyopo wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Padri Godian Simpinge katika maadhimisho ya ibada ya jumatano ya majivu yaliyofanyika Parokiani Bahi yakihudhuriwa na waumini wa Parokia hiyo waliofika kwa ajili ya kupaka majivu kama ishara ya kuianza safari ya siku 40 za kufunga na kujitakasa kiroho kabla ya ufufuko wa Yesu kristo siku ya Pasaka.
Amesema tendo la kupakwa majivu ni kuwakumbusha kuwa mwanadamu ni dhaifu aliyeumbwa kwa mavumbi na katika mavumbi atarejea kupitia kifo hivyo ni vema Mwanadamu kumtumikia Mungu maisha yake yote na kuachana na mambo ya duniani ambayo ipo siku atayaacha.
“ Tunapakwa majivu kama ishara ya mwanzo wa kipindi kipya cha kanisa kipindi cha kwaresma, kipindi cha toba cha siku arobaini, ambacho kinatutaka tutubu na kuiamini injili ya bwana wetu Yesu kristo na kwa kupitia toba hiyo tutaingizwa katika ufalme wa Mungu”. Amesema Simpinge.
Amewaasa waumini kufanya toba ya kweli kwa kudhamiria kuacha kurudia katika dhambi wanazozitubu ili kujipatanisha moja kwa moja na mwenyezi Mungu na kuepuka kuwa vigeugeu kwa kutubu huku wakiwa hawana dhamira ya kuachana na dhambi walizotubu kwani haitawajenga wao kiroho.
Tumtegemea Mungu na kuiamini ijili ya kristo, lazima tusali mpaka tuvuke na kupata majibu ya mahangaiko yetu’. Amesema Simpinge.