Dodoma FM

Serikali yatoa ruzuku kwaajili ya kupunguza bei ya mafuta

10 May 2022, 3:57 pm

Na;Yussuph Hassan.

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Serikali imetoa ruzuku ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta nchini.

Akiwasilisha taarifa ya serikali leo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ruzuku hiyo inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22 na haitagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea.

.

Ameongeza kuwa hatua nyingine zisizo za kifedha zinazochukuliwa na Serikali ili kuleta unafuu wa bei za mafuta ni pamoja na Kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo na Kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Bei za mafuta (Fuel Price Stabilization Fund).

.

Serikali imetoa fedha shilingi bilioni 100 kupunguza makali ya kupanda kwa bei ya mafuta, hiyo ikiwa ni hatua ya muda mfupi kwa mwezi Juni na kuongeza kuwa ifikapo mwaka wa fedha 2022/23, nafuu zaidi itapatikana kwani serikali imeshaomba mkopo wa masharti nafuu Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani ili kuleta nafuu ya bei ya mafuta nchini.