Shule shikizi kilio cha wananchi wengi vijijini
6 April 2022, 3:39 pm
Na; Victor Chigwada.
Changamoto ya usajili wa shule shikizi imekuwa kilio Cha maeneo mengi nchini licha ya kuwa shule hizo zimekuwa zikijengwa kwa lengo la kupunguza umbali kwa wanafunzi au kupunguza idadi ya wanafunzi kwa shule mama.
Kijiji cha Mima Wilayani Mpwapwa ni miongoni mwa vijiji vilivyo chukua hatua ya kujenga majengo ya shule shikizi lakini kwa muda mrefu wamekosa usajili wa shule hiyo.
Baadhi yao wakizungumza na taswira ya habari wamesema kuwa lengo ilikuwa ni kukabiliana na umbali wa shule ilipo kutoka kitongoji cha Makawila kwani wanafunzi hutembea umbali mrefu.
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Mima Bw.Ameli Mtuli ameeleza kuwa usajili wa shule hiyo ungesaidia kupunguza changamoto ya umbali kwa wanafunzi na kuiomba Serikali kuwasaidia kutatua adha hiyo.
Aidha naye Diwani wa Kata Mim@ Bw.Bezaeli Mnyambwa amesema kuwa licha ya hayo lakini pia uchakavu wa shule mama bado ni changamoto ambako nako kunahitaji ukarabati.
Mnyambwa ameongeza kuwa kwa Sasa wanaendelea na utatuzi wa kuongeza vyumba vya madarasa pamoja na ujenzi wa shule shikizi ili kukabiliana na umbali mrefu kwa wanafunzi.
Usajili wa shule shikizi umekuwa ukizingatia mazingira bora na rafiki kwa mwanafunzi lakini pia usafi na usalama wa wa afya ya mwanafunzi.