Dodoma FM

Serikali yaombwa kufanya ukarabati katika shule kongwe za msingi

7 March 2022, 12:43 pm

Na; Mariam Matundu.

Serikali imeombwa kufanya ukarabati wa majengo katika shule kongwe za msingi ili kukabiliana na changamoto ya uchakavu wa majengo unaoathiri ufundishaji hasa kwa watoto wenye ulemavu.

Shule ya msingi Iboni iliyopo wilayani Kondoa ni miongoni mwa shule kongwe inayotoa elimu jumuishi ambapo moja ya jengo lililojengwa tangu mwaka 1952 limebomolewa na kusababisha adha kubwa kwa wanafunzi wenye ulemavu wasioona na wenye ulemavu wa akili.

Akizungumza na taswira ya habari mwalimu mkuu wa shule hiyo Fabian Charles amesema waliamua kubomoa jengo hilo kwa kuhofisia linge bomoka na kuleta madhara kwa wanafunzi hao .

Amesema hatua hiyo inasababisha changamoto kwa wanafunzi wasioona kwa kuwa kifusi ni kikubwa na pia inawalazimu kuwachanganya wanafunzi hao na wanafunzi wenye ulemavu wa akili katika darasa moja.

Taswira ya habari imezungumza na wananchi wa kata ya iboni mahali ilipo shule hiyo kutaka kujua ni upi wajibu wao kuhakikisha wanaondoa kifusi hicho ambacho ni kikwazo kwa wanafunzi wenye ulemavu.

Juma Saidi Jobisho ni mwenyekiti wa mtaa wa Iboni amesema tayari wamefikisha taarifa hizo kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo na kuahidi kwamba atashughulikia suala hilo mapema iwezekanavyo.

Serikali inaandaa bajeti kwa ajili ya awamu ya pili ya ukarabati wa shule kongwe ambao utahusisha nyumba za walimu pamoja na majengo mengine kwa lengo la kuwawezesha watumishi kuishi katika mazingira bora na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.