Serikali yatarajia kuzindua ujenzi wa ofisi za wizara awamu ya pili
30 November 2021, 12:34 pm
Na; Mariam Matundu.
Serikali inatarajia kuzindua ujenzi wa ofisi za Wizara awamu ya pili zinazojengwa katika mji wa Serikali pamoja na uzinduzi wa huduma za kijami ikiwemo uwekaji wa jiwe la msingi kituo cha polisi chenye hadhi ya daraja la kwanza .
Hayo yanatarajiwa kufanyika wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 60 ya huru Dec. 2 mwaka huu zitakazofanyika katika mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma .
Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema kuwa pamoja na hayo pia kutafanyika ukaguzi wa barabara za lami za mji wa Serikali zenye urefu wa Km 51.2 ambazo ujenzi wake umefikia zaidi ya 85%.
Amesema kuanzia Nov. mosi Serikali ilitoa muongozo wa kufanyika kwa shughuli mbalimbali za maendeleo, uchumi na biashara, michezo na kijamii ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo hadi kufikia siku ya kilele Dec. 9 .
Pamoja na hayo ameliagiza jeshi la Polisi usalama barabarani Mkoani hapa kuruhusu daladala za kubeba abiria kutoka viunga mbalimbali vya Jiji la Dodoma kupeleka na kuchukua abiria kwenye eneo la mji wa Serikali mtumba.
Mgeni rasmi katika sherehe hizo za uzinduzi anatarajiwa kuwa Waziri mkuu wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa huku kauli mbiu ikiwa ni MIAKA 60 YA UHURU TANZANIA IMARA KAZI IENDELEE.