Wizara ya Ulinzi imesema itaendelea kuhakikisha nchi inakuwa salama
29 November 2021, 1:33 pm
Na; Mindi Joseph.
Wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa imesema itaendelea kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi inakuwa salama huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa nchi.
Akizungumza leo jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax amesema jukumu la wizara hiyo ni kuhakikisha JWTZ inataekeleza majukumu yake kikamilifu ikiwa ni pamoja na ulinzi wa mipaka ya jamhuri ya muungano.
Ameongeza kuwa wananchi wanawajibu wa kushiriki katika ulinzi wa nchi kwa kujitoa pamoja na kutoa taarifa za viashiria vya matisho ya kiulinzi na kiusalama.
Aidha Dkt. Stergomena amesema wizara hiyo imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya wanajeshi kote nchini.
Katika hatua nyingine Dkt. Stergomena amevipongeza vyombo vya habari nchini na kuvitaka kuendelea kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na utulivu uliopo katika tasnia hiyo.