Viongozi wa skimu za umwagiliaji wametakiwa kusimamia zoezi la kutunisha mfuko wa umwagiliaji
28 October 2021, 11:17 am
Na;Mindi Joseph.
Mhandisi wa Umwagiliaji amewataka viongozi katika Skimu za Umwagiliaji kusimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji ada na tozo kwa lengo la kutunisha mfuko wa Umwagiliaji.
Akizungumza na Taswira ya habari kutoka Mkoani Iringa Mhandisi wa Umwagiliaji Onesmo Kahoggo amesema endapo wakulima katika Skimu za Umwagiliaji watachangia fedha za ada ya usajili na matunzo kwa wakati, itasaidia kuharakisha ukarabati wa Skimu zilizoharibika kutokana na athari zitokanazo na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kujenga Skimu mpya nchini.
Ametolea mfano zoezi la kuurejesha mto Ruaha Mdogo katika njia yake ya asili limegharimu fedha kutoka mfuko wa Umwagiliaji ambao unahitaji kuwezeshwa na wakulima hao.
Awali akiongea Diwani wa kata ya Ilolo Mpya Bw, Funda Mihayo amemshukuru Mkurugenzi wa Tume ya taifa ya Umwagiliaji Bw, Daudi Kaali kwa kuwezesha wataalamu wa tume kurekebisha miundombinu ya mifereji ya kupeleka maji katika mashamba ya wakulima.
Kwaupande wake Bi, Katarina Rashidi Mlaga mkulima mkazi wa kijiji cha Magozi ameishukuru serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kazi kubwa iliyofanya wa kurejesha mto Ruaha Mdogo katika njia yake ya asili, nakusema kuwa wakulima katika kijiji hicho hutegemea Zaidi kilimo cha umwagiliaji, na wamepata elimu ya kutosha kuhusu uchangiaji wa tozo za umwagiliaji na wapo tayari kuchangia.