Asasi za kiraia nchini zimetakiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa sensa
28 October 2021, 7:39 am
Na;Mindi Joseph.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anne Makinda ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge amezitaka Asasi za Kirai nchini kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa sensa kufuatia kuwepo upotoshaji wa sensa kuhusiana na chanjo ya Uviko 19.
Akizungumza katika Mdahalo wa AZAKI Mh Anne Makinda amesema AZAKI zisaidie kuelimisha Jamii kuhusu umuhimu wa sensa na kuondoa upotoshaji kwani sensa haina uhusiano na chanjo ya Uviko 19.
Ameongeza kuwa Wanaendelea na zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabiwa Watu Nchi nzima na wamekamilisha zoezi la Sensa ya majaribio iliyohusisha Mikoa 18 iliyoanza Mwezi wa 8 na kukamilika Mwezi wa 9.
Kwa upande wake Mtakwimu Mwandamizi,Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) David Mwaipopo amebainisha kuwa Tofauti ya Sensa ya mwaka 2022 na miaka mingine wametenga maeneo ya kuhesabiwa Watu hadi ngazi ya kitongoji kwa Vijijini na ngazi ya mtaaa kwa Mijini na sensa itawapatia idadi ya Watu na Hali zao.
Sensa ya watu na makazi imepangwa kufanyika ifikapo Agosti mwaka 2022 na wananchi wamehimizwa kuhakikisha wanahesabiwa ili Nchi ijue mahitaji ya wananchi kwani sensa itazingatia mahitaji ya wananchi.