Kata ya Mtanana yahitaji huduma ya maji katika kijiji chake cha Soiti
7 October 2021, 12:31 pm
Na ;Benard Filbert.
Licha ya uwepo wa Vijiji vitano katika Kata ya Mtanana Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma imeelezwa bado kijiji kimoja kinakabiliwa na ukosefu wa mradi wa maji kwa wakazi wa eneo hilo.
Hayo yameelezwa na diwani wa Kata ya Mtanana Bw. Joel Shedrack wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Kata hiyo.
Amesema kuwa Kata ya Mtanana ina Vijiji vitano huku Vijiji vinne vina miradi ya maji lakini Kijiji kimoja cha Soiti hakina huduma ya maji na hivi sasa kipo katika mpango wa utekelezaji wa mradi huo.
Kadhalika amesema kuwa katika visima vilivyopo kulikuwa na changamoto ya kuharibika kwa miundombinu na ilichangia kupungua kwa upatikanaji wa huduma ya maji hivyo wanaangalia namna bora ya kurekebisha miundombinu hiyo.
Hata hivyo ameitaka kamati ya maji ambayo inahusika na uuzaji wa maji kuhakikisha wanatunza fedha ili kutimiza malengo ya makubaliano ya fedha hizo ikiwemo kutekeleza miradi mingine ya maendeleo katika Kata ya Mtanana.