Kamati za ulinzi na usalama wa mtoto zatakiwa kuimarishwa ili kukabiliana na vitendo vya ukatili
6 October 2021, 1:11 pm
Na; Selemani Kodima.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameagiza kuimarishwa kwa Kamati za ulinzi na usalama wa mtoto ili zitumike kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Mh. Mwanaidi ametoa agizo hilo Mkoani Mbeya wakati akizungumza na Kamati za ulinzi wa mwanamke na mtoto pamoja na kikundi cha malezi chanya zinazotekeleza Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili wa Wanawake na watoto katika Halmashauri ya Mbeya
Akitoa taarifa ya MTAKUWWA kwa niaba ya wenzake Bw. Fransisco Mgwira amesema wamefanikiwa kupunguza vitendo vya ukatili kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine ikiwemo uongozi wa Kata.
Mhe. Mwanaidi pia ametoa wito kwa mamlaka zinazosimamia kesi za ukatili dhidi ya watoto na wanawake kusimamia uharakishaji wa kesi hizo na waathirika wapate haki zao.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema kesi hizo za ukatili zikiachwa muda mrefu zinapoteza ushahidi hivyo wahusika wanakosa haki zao zinazostahili na kuzidi kuathirika kisaikolojia na kufanya jitihada za kutokomeza vitendo hivyo kusuasua.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Mwanaidi amewataka wazazi kushirikiana katika malezi na kuwajibika ili kuwalinda watoto kutofikia hatua ya kukinzana na Sheria.