Jamii na wazazi washauriwa kuwafundisha watoto maadili na tamaduni za kitanzania
28 September 2021, 1:04 pm
Na;Thadei Tesha.
Viongozi kwa kushirikiana na wazazi wameshauriwa kuwa mstari wa mbele katika kuwafundisha watoto wao maadili na tamaduni za kitanzania ili kukuza kizazi cha watoto wenye kufuata misingi na tamaduni nzuri za kitanzania.
Akizungumza na taswira ya habari afisa utamaduni wa jiji la Dodoma Bw Desderi kusenza amesema kwa sasa utamaduni wa kitanzania umeathiriwa na utandawazi pamoja na mila na desturi za kimagharibi ambazo zimekuwa zikileta athari ambapo amesema ofisi yao imeandaa mikakati kwa ajili ya kuhakikisha tamaduni nzuri za kitanzania zinapewa kipaumbele kwa kuandaa matamasha pamoja na maonyesho ya sanaa mashuleni.
Aidha Bwn Kusenza amewataka vijana nchini kuacha kuiga tamaduni mbaya za kimagharibi ambazo zimekuwa zikileta athari za mmomonyoko wa kimaadili katika jamii na badala yake kuwa mstari wa mbele kulinda mila na desturi nzuri za kitanzania.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi jijini hapa wametoa wito kwa viongozi kuwawezesha kwa kuwapa hamasa watu mbalimbali walio mstari wa mbele katika kulinda utamaduni kupitia sanaa na maonesho mbalimbali.
Suala la utamaduni pamoja na mila za kitanzania limeendelea kuathiriwa na mtindo wa maisha ya kimagharibi ambapo jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupambana na mila na desturi potovu.