Mlali bondeni waendeleza jitihada za kutatua changamoto za miundombinu ya daraja
27 September 2021, 11:56 am
Na ;Selemani Kodima.
Uongozi wa kijiji cha Mlali bondeni wilayani Kongwa umesema unaendelea kuchukua jitihada za kutatua changamoto ya miundombinu ya daraja linalounganisha mlali – chibarau ili kusaidia kupunguza matukio ya ajali katika eneo hilo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kijiji cha Mlali Bondeni Bw. Peter Mpanga ambapo amesema daraja hilo limekuwa likitumiwa zaidi na wanafunzi wa shule ya msingi chibarau licha ya uwepo wa matukio ya ajali za mara kwa mara za watu kudondoka katika daraja hilo.
Amesema jitahada ambazo wamechukua za kuboresha daraja hilo ni ushirikiano wa Uongozi wa kijiji na wananchi wa kijiji cha Mlali bondeni.
Bw. Mpanga amesema taarifa ya Ubovu wa daraja hilo wamekuwa wakizitoa katika Vikao vya kijiji ,kata ,mpaka wilaya huku majibu ya utatuzi wa miundombinu hiyo ukiwa bado changamoto.
Hata hivyo Daraja la Mlali bondeni limeripoti kuwa na matukio ya ajali ambazo zimekuwa zikihusishwa watu kuangua na kusababisha vifo.