Wilaya ya Kongwa yaja na mkakati wa kulima mashamba yote ya shule za sekondari na msingi
13 September 2021, 1:35 pm
Na; Beanard Filbert.
Mkuu wa wilaya ya Kongwa Remidius Emannuel amesema wilaya hiyo imeweka mkakati wa kulima mashamba yote ya shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo lengo ikiwa wanafunzi wote kupata chakula shuleni na kudhibiti tatizo la lishe Duni.
Amesema hayo wakati akizungumza na taswira ya habari baada ya kusaini mkataba na mkuu wa mkoa wa Dodoma Antony Mtaka wa kuimarisha lishe bora katika maeneo yote ya mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Remidius amesema mkakati uliopo katika wilaya ya kongwa ni kulima mashamba yote ya shule ya msingi na sekondari ambayo yalikuwa wazi hali itakayosaidia kuzalisha mazao mengi ya chakula ambayo yatasaidia wanafunzi wote kula shuleni.
Ameongeza kuwa wanaendelea kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuimarisha lishe bora katika wilaya ya Kongwa likiwepo shirika la world vision ambalo linatekeleza mradi wa FAMILIA BORA katika baadhi ya kata.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bahi Mwanahamis Mkunda ameiambia taswira ya habari kuwa mkakati walionao ni kuhakikisha kila shule wanapata chakula kupitia miradi yao ikiwepo ya ufugaji wa mbuzi na ng’ombe wa maziwa pamoja na kuelimisha jamii umuhimu wa kupika chakula chenye lishe bora.
Hivi karibuni mkuu wa Mkoa wa Dodoma aliwasainisha wakuu wa wilaya zote za Dodoma mkataba wa miaka 5 wa kuimarisha lishe bora katika maeneo yao mradi ambao unafadhiliwa na nchi ya marekani USAID kupitia shirika la SAVE THE CHILDREN.