Baadhi ya vijana walalamikiwa kushindwa kurudisha mikopo inayotolewa na halmashauri
26 August 2021, 1:00 pm
Na; Benard Filbert.
Licha ya Serikali kupitia Halmashauri mbalimbali Nchini kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali imeelezwa kuwa moja ya changamoto kubwa ni baadhi ya vijana kushindwa kurudisha mikopo hiyo.
Hayo yameelezwa na afisa maendeleo Jiji la Dodoma Bw. Daniel Manyama wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu mwenendo wa marejesho ya mikopo ambayo inatolewa na Halmashauri.
Bw. manyama amesema pamoja na juhudi za Serikali kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali bado kuna changamoto kutokana na baadhi yao kutokuwa waadilifu katika kurudisha mikopo hiyo ili iwasaidie watu wengine.
Amesema awali kanuni zilikuwa haziruhusu kumshtaki mtu yeyote au kikundi kilichokopa lakini hivi sasa zimefanyiwa marekebisho na yeyote atakaye kaidi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Baadhi ya vijana wamesema ni vyema halmashauri zikaangalia namna bora ya kukusanya pesa hizo ili ziweze kuwasaidia wahitaji wengine ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu ya namna bora ya kutumia fedha hizo baada ya kukopa.
Kuanzia mwaka 2016 hadi sasa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa mkopo kwa vijana pekee kiasi cha shilingi Billion mbili, milion miatisa kumi na sita huku mkopo wa fedha hizo ukiwa bado haujarudishwa mpaka hivi sasa.