RUWASA yatatua kero ya maji Masinyeti iliyo dumu kwa miaka ishirini
22 July 2021, 3:35 pm
Na; Benard Filbert.
Wakala wa maji vijijini RUWASA katika wilaya ya Kongwa wamefanikiwa kuchimba kisima cha maji katika kijiji cha masinyeti ambacho kitasaidia kuondoa changamoto ambazo wakazi hao walikuwa wakikutana nazo ikiwepo kutembea umbali mrefu kufuata maji.
Hayo yameelezwa na meneja wa wakala wa maji wilaya ya Kongwa mhandisi Kaitaba Lugetulila wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kijiji cha masinyeti wilayani humo.
Mhandisi kaitaba amesema mpaka hivi sasa wamefanikisha kuchimba kisima kikubwa ambacho kitakidhi huduma ya upatikanaji wa maji katika kijiji cha masinyeti huku zoezi linalofuata hivi sasa ni kujua uwezo wa uzalishaji wa maji katika kisima hicho.
Ameongeza kuwa kwa utafiti walioufanya katika kisima hicho maji hayo yatakidhi matumizi ya wakazi hao kwa takribani miaka 20.
Amewaomba wakazi wa kijiji cha masinyeti kutoa ushirikiano kwa wafanyakazi wa RUWASA ambao wataanza kutekeleza mradi huo mwezi wa nane ili kufanisha haraka bila vikwazo.
Hayo yanajiri kufuatia hivi karibuni wakazi wa kijiji cha masinyeti kata ya Iduo wilaya ya Kongwa kunukuliwa wakieleza changamoto zinazowakabili kutokana na ukosefu wa huduma ya maji.