Shule zinazotoa elimu jumuishi zaiomba serikali kuboresha miundombinu
16 July 2021, 1:12 pm
Na; Mariam Matundu.
Walimu wanaofundisha shule zinazotoa elimu jumuishi katika Wilaya ya Bahi na Dodoma mjini wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya shule zao ili kuwezesha watoto wenye mahitaji maalumu kujifunza vizuri.
Wamesema suala la uchache wa vyumba vya madarasa linasababisha darasa kuwa na wanafunzi wengi kuliko wastani unaotakiwa hali ambayo inawawia vigumu walimu hao kuwasaidia wanafunzi kuelewa kwa urahisi hasa watoto wenye ulemavu wa afya ya akili .
Afisa elimu kata ya Nkuhungu jijini Dodoma Bi. Salma Selemani amesema suala la mtaala bado ni changamoto kubwa kwa elimu jumuishi pamoja na upatikanaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ikiwemo kamusi ya lugha ya alama na vitabu vya nukta nundu.
Akijibia changamoto hizo mkurugenzi wa elimu maalumu TAMISEMI Julius Migeha amesema katika kutatua changamoto hizo serikali imefanya uchunguzi kwa watoto wote kabla ya kuandikishwa darasa ya kwanza mwaka huu ili kuwatambua wenye ulemavu na mahitaji yao katika shule zao ili waweze kutatua changamoto hizo.
Suala la utoaji wa elimu jumuishi katika shule mbalimbali bado linakabiliwa cha changamoto nyingi zinazokwamisha elimu hiyo kutolewa kwa ufanisi.