Moleti waiomba Serikali kuwapelekea huduma ya umeme
13 July 2021, 1:20 pm
Na; Benard Filbert.
Wakazi wa Kijiji cha Moleti Wilaya ya Kongwa wameiomba Serikali kuharakisha kuwaunganishia huduma ya umeme wa REA kutokana na kuchangishwa fedha takribani mwaka mmoja uliopita.
Wamesema hayo wakati wakizungumza na Dodoma fm ambapo wamedai kuwa baadhi ya Vijiji vimefikishiwa huduma ya umeme kwa haraka lakini kwao kumekuwa na sintofahamu.
Bw.Shukuru Nhembo ni mkazi wa Kijiji cha Moleti ameiambia taswira ya habari kuwa katika Kata hiyo kuna baadhi ya maeneo umeme umefika lakini katika Kijiji chao bado huduma hiyo haipo.
Taswira ya habari imezungumza na kaimu mtendaji wa Kijiji cha Moleti Bw.Luca Muhando ambaye amekiri wananchi kuchangishwa fedha mwaka mmoja uliopita lakini hawaoni dalili za kuletewa umeme.
Taswira ya habari inaendelea na jitihada za kumtafuta meneja wa Shirika la umeme tanesco wilaya ya Kongwa ili kujibia changamoto hiyo.