Ukosefu wa maji safi na salama waathiri uchumi wa kijiji cha Asanje
29 June 2021, 11:21 am
Na; Benard Filbert.
Ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika kijiji cha Asanje wilayani bahi imetajwa kuathiri shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa kijiji hicho.
Hayo yameelezwa na wakazi wa kijiji hicho wakati wakizungumza na taswira ya habari ambapo wamesema kuwa upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho imekuwa ndoto isiyotimia na hivyo kuwa changamoto kubwa.
Wakizungumzia maji wanayotumia hivi sasa wamesema wanachota katika visima lakini hayana usalama kwa matumizi ya binadamu.
Juma Dobogo ni mwenyekiti wa kijiji cha asanje amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku akisema wananchi wanasita kutoa michango kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Babayu bwana Hussein Kamau amesema katika kutatua changamoto hiyo serikali imetenga bajeti kiasi cha milioni 200 kupitia wakala wa maji vijijini RUWASA na hivi karibuni utekelezaji utaanza.
Changamoto ya upatikanaji wa maji imekuwa ikikumba vijiji vingi nchini huku serikali ikijitahidi kutatua kero hiyo.