Ubovu wa barabara katika kata ya Ovada umepelekea baadhi ya akina mama wajawazito kujifungulia njiani
21 June 2021, 11:03 am
Na; Benard Filbert.
Changamoto ya miundombinu ya barabara katika kata ya Ovada wilayani Chemba imetajwa kuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo .
Hayo yameelezwa na wakazi wa kata hiyo wakati wakizungumza na taswira ya habari ambapo wamesema kuwa ubovu wa miundombinu ya barabara imekuwa changamoto kubwa katika kata hiyo.
Jumanne Issa ni mkazi wa kata hiyo ameiambia taswira ya habari kuwa kuna baadhi ya wanawake wajawazito wanalazimika kujifungulia njiani kutokana na barabara kutokupitika kirahisi.
Diwani wa kata ya Ovada akizungumza na taswira ya habari amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku akisema barabara zote zinazounganisha vijiji katika kata hiyo haziridhishi.
Amesema hatua ndogo walizochukua mpaka hivi sasa ni kushirikisha wananchi kufanya marekebisho huku wakisubiri bajeti kutoka TARURA kuanzia mwezi wa saba.
Ubovu wa miundombinu ya barabara imekuwa changamoto kubwa katika baadhi ya maeneo nchini huku ikipelekea baadhi ya wananchi kukosa huduma za kijamii.