Waziri Gwajima atoa siku 30 kwa kamati ya mpito kufanikisha uchaguzi mkuu wa mashirika yasiyo ya kiserikali
7 June 2021, 12:37 pm
Na; Mariam Matundu.
WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii,jinsia Wazee na watoto Dkt.Dorothy Gwajima ametoa siku 30 kwa kamati ya mpito kufanikisha uchaguzi mkuu wa baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuzingatia hadidu rejea zitakazotolewa kwa kazi hiyo.
Waziri Gwajima ametoa tamko hilo leo jijini dodoma na kuitaka kamati ya mpito katika kuelekea kufanikisha uchaguzi mkuu wa Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO) kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa kifungu cha 25(1) cha sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali kuwa kifungu cha 25(2) cha sheria hiyo baraza ni mwamvuli kwa mashirika yote yaliyosajiliwa Tanzania Bara.
Aidha waziri Gwajima ameunda kamati ya mpito ya mashirika yasiyo ya kiserikali ili kufanikisha uchaguzi unafanyika haraka kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi zilizopo ambapo kamati iliyoundwa itakuwa na wajumbe kumi(10).
Baraza linatakiwa kufanya uchaguzi wa viongozi wa wajumbe wa baraza kila baada ya miaka mitatu ambapo baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali mara ya mwisho lilifanya uchaguzi wake mwaka 2016 kwa kanuni za uchaguzi.