Wafugaji wilayani Chemba walia na changamoto ya kukosa soko la kuuzia mifugo yao
3 June 2021, 12:11 pm
Na;Victor Chigwada.
Wakulima na wafugaji wa Kata ya Farkwa katika Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma wameiomba Serikali kuwatatulia changamoto ya soko la mazao pamoja na majosho ili wafanye shughuli zao kwa tija.
Wakizungumza na taswira ya habari wananchi hao wamesema kuwa wanashindwa kuzalisha mazao kwa wingi kutokana na ukosefu wa soko huku kwa upande wa mifugo ikikabiliwa na magonjwa mbalimbali kwa kukosa majosho.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bubutole Bw. Hosea Ndalami amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuiomba Serikali kuwatafutia soko la uhakika pamoja na kuwajengea majosho ya kutosha ili wazalishe kwa wingi.
Naye Diwani wa Kata ya Farkwa Bw.Stephani Patrick amesema upande wa kilimo licha ya kukosa soko lakini pia ukosefu wa nyenzo za kulimia, mbegu na elimu ya kilimo bado ni changamoto kwa wakulima.
Kwa upande wa wafugaji Bw. Patrick amesema pamoja na jitihada anazofanya lakini bado wafugaji wanakabiliwa na ukosefu wa majosho na dawa kwa ajili ya kutibu wadudu wanaoshambulia mifugo yao na Kata nzima lipo moja tu.
Uwepo wa majosho ya kuogeshea mifugo unatajwa kuwa utasaidia kuwaepusha wafugaji kuingia gharama za kununua madawa kwa ajili ya mifugo yao.