Mradi wa Bomba la mafuta utasaidia kuongeza pato la Taifa .
20 May 2021, 2:06 pm
Yussuph Hans
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan, amesema mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga utasaidia kuvuta Wawekezaji Ukanda wa Afrika Mashariki, kuongeza ajira pamoja na pato la Taifa.
Amebainisha hayo katika hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Ujenzi wa bomba la Mafuta la Afrika Mashariki kati ya Uganda na Tanzania, uliofanyika Ikulu Jijini Dar es salam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mh.Rais Samia Suluhu amesema mradi huo umepita katika Mikoa Minane na Wilaya 28, ambapo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha ajira kwa Watanzania, kuongezeka kwa mapato ya kodi kwa 60% pamoja na kuchochea shughuli za biashara ya mafuta na gesi.
Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kukamilika kwa mradi huo, kutakuza sekta mbalimbali za biashara, viwanda na kilimo nchini Uganda, pamoja na kuboresha miundimbinu na huduma za kijamii.
Akifafanua namna mradi huo utakavyotekelezwa, Waziri wa Nishati Mh. Medard Kalemani amesema ni ujenzi wa bomba lenyewe, kujenga vituo kwa ajili ya kusukuma mafuta, kujenga vituo vya kulainisha mafuta na kujenga vituo vya kufunga valvu ambapo kwa kiasi kikubwa mradi huo utainufaisha Tanzania kimapato.
Hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kati ya Tanzania na Uganda umefanyika leo ikulu jijini dar es salam kuwakilishwa na Marais wa pande zote mbili pamoja na viongozi mbalimbali huku ikishirikisha kampuni ya Total ya Ufaransa, Shirika la maendeleo ya petrol tanzania Tpdc, na Kampuni ya Sinok ya China.